KITAIFA

Watu Watatu Wapandishwa Kizimbani Kwa Tuhuma Za Mauaji Ya Watoto Njombe

on

Washukiwa watatu wa utekaji na mauaji ya watoto wa chini ya miaka 10 wilayani Njombe, kusini magharibi mwa Tanzania wamepandishwa mahakamani hii leo.

Watuhumiwa hao waliowekwa wazi kwa mara ya kwanza hii leo ni Nasson Kaduma, Joel Nziku na Alphonce Danda.Wote wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe.

Gazeti la Mwananchi linaripoti kuwa Nje ya mahakama hiyo ulinzi mkali wa polisi umeimarishwa na msafara wa watuhumiwa hao ukisindikizwa na magari sita ya polisi.

Watoto takribani 10 wameshauawa toka visa hivyo vya kutamausha kuanza kuripotiwa mwezi Disemba.

Miili ya watoto hao imekutwa ikiwa imenyofolewa baadhi ya viungo kama matumbo, vidole, pua na macho. Wauaji hao pia wamekuwa wakinyofoa viungo vya siri vya watoto hao.

Mamlaka nchini Tanzania zimekuwa zikihusisha mauaji hayo na imani za kishirikina, waganga wa kienyeji wanalaumiwa kwa kuwaaminisha watu kuwa viungo vya binaadamu vinavuta bahati na utajiri.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Ijumaa aliliambia Bunge kuwa tayari watu 29 wameshakamatwa kutokana na matukio hayo, na kusema kuwa uchunguzi bado unaendelea.

Miongoni mwa waiokamatwa ni wafanyabiashara maarufu wa eneo hilo pamoja na waganga wa jadi.

 

TOA MAONI YAKO HAPA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *