KITAIFA

Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa Kupelekwa kwa rais magufuli

on

Hatimaye Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa Tanzania umepitishwa na Bunge la nchi hiyo na sasa utapelewkwa kwa Rais Magufuli ili ausaini na kuwa sheria.

Upitishwaji wa muswada huo umepitia vigingi kadhaa, ukikosolewa vikali na vyama vya siasa vya upinzani na asasi za kiraia ambao wanadai utaminya demokrasia nchini humo.

Hata hivyo wabunge wa chama tawala cha CCM ambao ni wengi Zaidi wameutetea muswada kwa kudai unaenda kusafisha siasa za vyama vingi.

Baada ya kupita bungeni muswada huo unatarajiwa kusainiwa na rais Magufuli ambaye serikali yake imekuwa ikibeba lawama za kuminya upinzani na uhuru wa kujieleza.

Waziri kivuli na mbunge wa Bunda, kupitia Chadema Esther Bulaya ameuita muswada huo kuwa ni ‘uonevu mkubwa dhidi ya vyama upinzani.’

Uonevu kwa mujibu wa Bulaya unadhihiri kwa msajili wa vyama vya siasa kupewa mamlaka ya kuingilia mfumo wa uchaguzi ndani ya chama akisema kutapunguza uhuru wa vyama kufanya chaguzi bila mashinikizo kutoka ofisi ya msajili.

Uonevu mwengine kwa mujibu wa upinzani ni masharti ya namna ya utoaji wa elimu ya uraia kwa kuzuia vyama rafiki kutoka nje kushiriki.

“Ni haki yao ya msingi ya kueneza itikadi za vyama vyao bila kujali mipaka ya nchi…huu ni upungufu mkubwa kwani msajili anaweza kukataa tu kutokana na maslahi yake bila kuongozwa na sheria inayopendekezwa,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alilieleza Bunge kuwakuwa muswada huo ni kiboko.

Mhagama kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi ni amesema pamoja na mambo mengine muswada huo unalenga kumpa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakiki chama cha siasa wakati wowote.

“Lengo ni kuhakikisha chama cha siasa kinakuwa na sifa za usajili muda wote wa uhai wake na kueleza bayana mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kuhakiki muda wowote utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa ili kuhakikisha chama cha siasa kinazingatia na kutekeleza masharti ya usajili,” amenukuliwa na Mwananchi akisema.

Wakili Jebra Kambole amesema kuwa bado kuna ukakasi mkubwa hususani nguvu alizopewa msajili, “Watakaoanza kuathirika muswada ukianza kutekelezwa ni vyama vidogo (vya upinzani). Lakini pale msajili atakapotumia mamlaka yake ipasavyo vyama vingi vitaumia.”

Moja ya kifungu kinachopingwa ni cha Kifungu cha 19 ambacho kinasema msajili anaweza kukisimamisha usajili wa chama kwa sababu atakazozitaja na kwa muda atakaouweka mpaka ili chama hicho kiweze kujirekebisha.

Chama ambacho kimesimamishiwa usajili hakitaweza kufanya shughuli zote za kisiasa.Na iwapo msajili ataona chama hicho hakijajirekebisha anaweza kukifutia usajili.

Kifungu hiki, wapinzani wanadai kinaweza kutumika kuzuia vyama kushiriki uchaguzi kwa jusimamishiwa usajili kabla yay a uchaguzi na kurudishiwa usajili baada ya uchaguzi kupita.Awali vyama vya upinzani vilionesha kufurahishwa na baadhi ya mabadiliko yaliyoyofanywa na kamati ya bunge ya sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya vyama 15 vya upinzani, Jumapili Januari 27, 2019 jijini Dar es Salaam, naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu amesema baada ya kutoa maoni yao mbele ya kamati hiyo hivi karibuni bungeni Dodoma, hoja nyingi walizopigia kelele zimesikilizwa.

“Tulipigia kelele suala la mafunzo na adhabu zake. Kamati baada ya kupitia hoja zetu, kwanza imepunguza adhabu kutoka Sh1 milioni hadi Sh500,000 na jela kutoka miezi 6 hadi mitatu,” Mwalimualinukuliwa na Mwananchi.

Hata hivyo, alisema bado kuna utata umebaki wa kuchanganya elimu ya uraia na kujengeana uwezo ndani ya chama.

 

TOA MAONI YAKO HAPA

Recommended for you

Leave a Reply