KITAIFA

UJENZI WA KITUO CHA AFYA MANYIRE KATA YA MLANGARINI CHAKAMILIKA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 98%

on

Hatimaye zoezi la ujenzi wa miundombinu ya jengo la kituo cha Afya Manyire, kata ya Mlangarini, halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru, umekamilika kwa zaidi ya asilimia 98%, huku majengo hayo yakitegemewa kuanza kutumika muda mfupi kuanzia sasa.

Ujenzi wa jengo hilo la kituo hicho cha afya, ulianza kwa nguvu za wananchi wa Mlangarini kwa ufadhili mkubwa wa mheshimiwa diwani wao mstaafu mpaka kufikia hatua ya boma, ambapo umaliziaji na ukamilishaji wa jengo hilo, umefanyika kwa msaada mkubwa wa Ubalozi wa Japani nchini Tanzania kwa kutoa fedha, kiasi cha shilingi milioni 191.9, fedha zilizohusisha ukamilishaji wa miundombinu ya jengo hilo pamoja na ununuzi wa samani za ndani.

Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, amesema kuwa, ukamilishaji wa miundombinu ya kituo hicho cha afya, umechukua takribani miezi sita, kufikia hatua hiyo na tayari taratibu za kufungua kituo hicho zinafanyika ili wananchi waanze kupata huduma.

Naye Mhandisi wa Ujenzi, halmashauri ya Arusha, Mhandisi Bibie Manzi, amesema kuwa, kati ya fedha hizo zote, kiasi cha shilingi milioni 143.9 kimetumika kufanya shughuli mbalimbali za umaliziaji wa miundombinu ya jengo hilo ikiwemo, usakafiaji wa kuta za jengo lote ndani na nje,  uwekaji  sakafu ya chini na kunakshi sakafu ya jengo kwa malumalu,  uwekaji wa dari, milango na madirisha pamoja na miundo mbinu yote ya maji na umeme, huku shilingi milioni 48 zinatumika kununua samani za ndani za jengo hilo ikiwemo vitanda vya wodi zote.

“Katika shilingi milioni 191.9 zilizotolewa na ubalozi wa Japani,kiasi cha shilingi milioni 143.9 zimetumika katika umaliziaji wa miundombinu ya jengo hilo na shilingi milioni 48 zinatumika kununua samani za ndani ikiwemo vitanda vya wodi zote na chumba cha upasuaji” amethibitisha Mhandisi

Mhandisi Bibie amefafanua kuwa jengo hilo ni jengo pacha ambalo majengo yameunganishwa likiwa limehusisha, jengo la wagonjwa wa nje (OPO),  wodi ya uzazi mama na mtoto (Maternity word), jengo la maabara, jengo la upasuaji (theatre) pamoja na  wodi za kulaza wagonjwa wa kawaida.

Mganga Mkuu, halmashauri ya Arusha Dkt. Petro Mboya, ameelezea kuwa kukamilika kwa kituo hicho afya cha Manyire kifanya halmashauri kuwa na jumla ya vituo vya vya afya 8 na kuendelea kufanikisha adhma ya serikali ya awamu ya tano ya kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kila kata kuwa na kituo cha afya chenye hadhi ya nyota tano.

Mganga mkuu huyo, ameongeza kuwa,  kituo hicho cha afya kinategemea kutoa huduma zote za wagonjwa wa nje ‘OPD’, huduma za vipimo, huduma za upasuaji, huduma za afya ya mama na mtoto,huduma za ushauri nasaha, pamoja na huduma ya kulaza  wagonjwa 56 kwa wakati mmoja.

Aidha kituo hicho cha afya, kinategemea kuhudumia zaidi ya watu elfu sita na kaya 1,200 zenye wastani wa watu watano kwa kila kaya wa kata ya Mlangarini na kijiji cha vijiji vya jirani vya kata ya Nduruma.

Awali chimbuko la mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Manyire, ulianza kwa kuibuliwa na wananchi  mwaka 2013, kutokana na uhaba wa huduma za afya kwa wananchi wa maeneo hayo huku,na kulazimika kutembea zaidi ya Kilomita 20 wakifuata huduma katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru au haosptali ya wilaya ya Tengeru.

NA, JOVIN -ARUSHA

EXTR NEWS:KAULI YA WAZIRI MKUU KWA WAKULIMA WA KOROSHO NCHINI

TOA MAONI YAKO HAPA

Recommended for you

Leave a Reply