KIMATAIFA

Nimwiza Meghan : Miss Rwanda Aliye Zua Swala La Ukabila

on

Nimwiza Meghan ndiye msichana aliyeteuliwa kuwa Miss wa Rwanda mwaka 2019.

Hata hivyo mchakato wa uteuzi wa Miss uligubikwa na kurushiana matamshi yenye ubaguzi wa kikabila baina ya Wahutu na Watutsi.

Baadhi ya wakereketwa wa makabila hayo walirushiana maneno makali kwenye mitandao ya kijamii kila upande ukivutia kwake, hali iliyosababisha tume ya nchi hiyo ya kupambana na itikadi ya mauaji ya kimbari kutoa onyo kali kwa wanaochochea mgawanyiko wa kikabila chini ya kivuli cha kumteua Miss Rwanda.

imwiza Meghan aliwashinda wasichana 15 walioshindana katika raundi ya mwisho.

Amevikwa taji la Miss Rwanda huku akibubujikwa na machozi na kwa furaha isiyo na kifani akawashukuru watu wote waliomuunga mkono wakiwemo pia wazazi wake:

Hatahivyo kwa mara ya kwanza katika historia ya kumteua Miss Rwanda , mchakato uliingia dosari ya swala la ukabila baina ya Wahutu na Watutsi.

Miongoni mwa wasichana 15 waliotinga raundi ya fainali, mmoja wao Josianne Mwiseneza alikuwa kutoka kabila la Wahutu na alifanya bidii kubwa kufika kwenye fainali hadi kuteuliwa kuwa Miss Popularity kwa kuchaguliwa na wengi kupitia ujumbe wa simu na kwenye mitandao ya kijamii.

aKuna wengi waliofurahia bidii zake kama msichana wa kijijini aliyejiamini kupita kiasi hadi kuwakilisha mkoa wake wa Magharibi na kutinga fainali.

Lakini wakereketwa wa kabila la Kihutu wengi wanaoishi nchi za nje walitumia fursa hii kupaaza sauti kuwa wakati umewadia kupata Umiss, kauli iliyofuatiwa na majibizano makali kutoka upande mwingine kwamba Umiss hautolewi kwa vigezo vya ukabila.

 

Kabla ya Nimwiza Meghan kuvikwa taji lake, jaji alikumbusha vigezo wanavyotumia kumteua malkia mrembo kuliko wengine:

”Ni mambo matatu muhimu tunayozingatia, kwanza ni mwenendo wao, jinsi wanaovyotembea ama kujionyesha hapa mbele ya jopo la majaji kwa kifupi maumbile na urembo wao kwa ujumla.Tunaangalia pia jinsi wanavyojieleza kwa maswali tunayowauliza, kuna wanaojiamini kwa kujibu, kuna wanaopaparika na wengine ambao wanatoa majibu yenye maudhui kamili. Hayo yote tunayazingatia kumchagua dada mrembo kuliko wote”

Awali tume ya taifa ya kupambana na itikadi za mauaji ya kimbari ilionya kuchukua hatua kali kuhusu waliotumia fursa ya kampeni za kutafuta miss Rwanda na kuchochea chuki za kikabila miongoni mwa wananchi wa Rwanda.

 

TOA MAONI YAKO HAPA

Recommended for you

Leave a Reply