KITAIFA

Uchaguzi Mwaka 2020 Ni Tundu Lissu vs Lowassa

on

Hatimaye mbunge wa jimbo la Singida Mashariki nchini Tanzania, Tundu Lissu ametangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).hivi karibuni Tundu Lissu alieleza kuwa ikiwa chama chake kitamuunga mkono na kumteua kama mgombea basi atakuwa tayari kuwania kiti cha Urais na kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao mwakani.

Tundu Lissu ni moja ya wanasiasa wa upinzani ambao walikuwa wanatajwa mara kwa mara kuwania nafasi hiyo mwakani, baada ya waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa kufanya hivyo mwaka 2015 mara baada ya kuhama CCM miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu.

Duru za kisiasa tangu mwaka 2016 zilidokeza kuwa Tundu Lissu huenda akawa miongoni mwa wagombea urais kwa tiketi ya Chadema, lakini vilevile kauli iliyowahi kutolewa na Lowassa kuwa atagombea tena uraisi mwaka 2020 ilizua mjadala na kuweka mizani nani alifaa kuwania nafasi hiyo kati ya wanasiasa waliomo kwenye chama hicho.

Duru za kisiasa zinaonyesha kuwa Chadema kila uchaguzi mkuu unapowadia kinakuwa na mgombea mpya katika nafasi ya urais.Uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 Chadema walimteua Freeman Mbowe kugombea urais na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Prof Ibrahimu Lipumba wa CUF na Jakaya Kikwete wa CCM aliyenyakua ushindi.

Mwaka 2010 Chadema walimteua Dkt Wilbroad Slaa ambaye alishika nafasi ya pili akibwagwa na Kikwete aliyekuwa akitetea kiti chake kwa awamu ya pili nay a mwisho.Uchaguzi wa 2015 Chadema walimpokea Lowassa kutoka CCM na kumpa tiketi ya kuwania urais, hata hivyo alibwagwa na rais wa sasa Dkt John Magufuli wa CCM.Historia katika hili inaonekana kuwa upande wa Lissu.

Mchuano wa Lissu na Lowassa

Kama Chadema wataendeleza utamaduni wao wa kutorudia wagombea kwenye nafasi ya urais katika uchaguzi ujao kama walivyofanya kwenye chaguzi mwaka za 2005, 2010 na 2015 itakuwa hasara kwa aliyekuwa mgombea wa chama hicho ambaye aliungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.

Tangu kumalizika uchaguzi wa mwaka 2015 hadi sasa, Lowassa amekaririwa mara mbili akizungumzia nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2020 bila kubainisha chama atakachotumia.

Lowassa aliweka wazi nia hiyo Januari 14 mwaka 2016, alipozungumza na wafuasi wake wanaojulikana kama ‘Timu ya Mabadiliko’ wa Soko la Kariakoo jijini Dar es salaam.

“Wale walio na nia ya kutaka kujua mustakabali wangu kisiasa nawaambia kwamba pamoja na kuwepo kwa mambo ya kutaka kunikatisha tamaa, lakini sitakata tamaa na nipo tayari kuwania urais na kushinda kwa kipindi kijacho cha mwaka 2020.” Alikaririwa na vyombo vya habari wakati huo.

Aidha, mwezi Julai mwaka 2017 Lowassa alirudia kauli yake na kusisitiza kuwa ataingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais ifikapo mwaka 2020. Tathmini hapa inaonyesha mchuano kati ya Lissu na Lowassa ni mkubwa mno.

Mtaji wa Lowassa

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC), mgombea wa CCM, Dkt.John Magufuli aliibuka mshindi baada ya kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46. Edward Lowassa wa Chadema alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.

Je mgombea mpya ataweza kufikia idadi hiyo ya kura kama ilivyokuwa kwa Lowassa? Kwa vyovyote huu ni mtaji mkubwa sana kwa Lowassa. Ni mtaji ambao Chadema watalazimika kuutathimini kwa kiasi kikubwa, kwamba wamtose Lowassa na kumteua mgombea mpya Tundu Lissu au mwanasiasa mwingine?

Mtihani huu wanaweza kuvuka kama Lowassa atakubali kuachwa kwenye kinyang’anyiro kisha kupendekeza mwanasiasa mwingine wa kuwania nafasi hiyo. Iwapo neno la Lowassa litakuwa nje ya Tundu Lissu utakuwa mtihani mwingine kwa Chadema na kauli hiyo itawaletea faida wafuasi wake.

Mtihani wa Tundu Lissu

Kiongozi mmoja wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) katika moja ya mkoa wa Kanda ya Ziwa ameambiwa mwandishi wa makala haya;

“Tundu Lissu ni mfano wa watu kama Dr.Slaa. Hana rasilimali fedha lakini ana watu nyuma yake wanaomkubali sana na ushawishi kwa siasa za upinzani. Lakini kwa nafasi ya urais sidhani kama atafanikiwa. Ndani ya chama wapo wanaomuunga Mkono lakini sio chaguo la mwenyekiti wala timu ya mwenyekiti.

“Na bado kuna suala ya ushirikiano na vyama vingine vya upinzani. Kama unaona harakati za Zitto Kabwe hadi sasa ni dhahiri anatamani sana angepata nguvu ya vijana na wanachama wa Chadema hasa kipindi hiki kuelekea kwenye chaguzi lakini kule ACT-Wazalendo hana wanachama wengi,”

Katika tathmini hiyo inaonyesha kuwa Tundu Lissu anatakiwa kuwahamasisha viajana wa Chadema, ikizingatiwa kuwa sasa ile hamasa imepoa, Mwenyekiti wao Freeman Mbowe yupo gerezani. Kwahiyo iwapo Tundu Lissu atafanikiwa kuwashawishi vijana hawa kwa vyovyote ni faida kwake, lakini akishindwa itakuwa hasara kubwa.

Hata kama haijatangazwa hadharani lakini duru za kisiasa zinasema kuwa mwanasiasa,waziri na mbunge wa zamani wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ni miongoni mwa majina yanayotikisa kwenye siasa za ndani za Chadema.

Duru za kisiasa zinamtaja Lazaro Nyalandu kuwa mtu wa karibu wa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa. Pia inaelezwa kuwa Nyalandu ndiye tegemeo la Lowassa iwapo ataachwa nje ya kinyang’anyiro cha kuwania urais.

Vilevile Lowassa mwenyewe licha ya kusema atagombea, hali inaonyesha kinyume chake kutokana na umri wake kumtupa mkono,ambapo mwaka 2020 atafikisha miaka 67, hivyo basi kisiasa ameandaa ‘mrithi’ wa kuwania nafasi hiyo.

Nguvu ya vikao vya Chadema

Katiba ya Chadema Ibara ya 7(7)(16), inaeleza moja ya kazi za Kamati Kuu ya chama hicho ni kufanya utafiti wa wagombea uraisi na mgombea mwenza na kuwasilisha ripoti yake Baraza Kuu, ambalo hupendekeza majina kwa mkutano ambao una mamlaka ya kuwateua.

Kwa msingi huo pamoja na tamko la Lissu bado haliwezi kumpa nafasi moja kwa moja kama mgombea anayekubalika.

Inawezekana pia tamko lake likawa hatua ya kwanza kupima upepo wakati Kamati Kuu ikiwa kwenye utafiti wa wanasiasa wenye sifa za kugombea urais ndani ya chama hicho pamoja na wagombea wenza. Hilo ni faida kwake.

Upande wa pili ni kwamba majina mawili ya Edward Lowassa na Tundu Lissu yapo hadharani kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Hivyo basi inategemewa kuibuka majina mengine Chadema, ambapo duru za kisiasa zinataja majina mawili ya Lazaro Nyalandu na waziri mkuu wa zamani Frederick Sumaye.

Kamati Kuu ya Chadema haiwezi kuyatosa majina ya Lissu, Lowassa, Nyalandu na Sumaye, ni lazima kati ya majina haya mmojawapo anaweza kukabidhiwa jahazi la Chadema kwenye uchaguzi ujao. Hilo litatokea iwapo hoja mbili zitasimamiwa; mgombea mpya au kurudia mgombea wa zamani.

Aidha, kinyang’anyiro hiki kinaibua hoja nyingine ya hatima ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambapo vyama vya upinzani vilishirikiana katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Umoja huo ulihusisha vyama vya Cuf, Chadema, NLD, TLP na NCCR-Mageuzi. Kwenye uchaguzi uliopita Lowassa alitoka Chadema, wakati mgombea mwenza alitoka chama Cuf, Juma Duni Haji. Chadema kama mshirika mama kwenye Ukawa, je watasimama peke yao au watarejesha muungano huo?

 

TOA MAONI YAKO HAPA

Leave a Reply