HABARI ZA MASTAR

Julius Mtatiro Atoa Yamoyoni Kuhusu Matokeo Ya Mtoto Wa Msani Wa Filamu Kajala

on

“Nimesoma maoni ya watu mbalimbali juu yako baada ya kupata divisheni IV kwenye CSEE. Baadhi ya watu wamekufanya kituko na kejeli, wamekufanya kuwa dhalili na usiye na akili. Baadhi wamesema huo ndiyo mwisho wako na wengine wamesema milango yako imefungwa.

Nilipita kwenye ukurasa mmoja wa Facebook wa mtu anayeheshimika sana akisema “ulizidiwa na umaarufu hewa”, wakati haya yakifanyika, wako mamia ya watoto wa watu maarufu wamefeli mtihani wa kidato cha nne na hawazungumziwi kabisa.

Kanuni za maisha zinaonesha, mtu anayesakamwa na kuzongwa kwa jambo dogo sana na linakuzwa na kuwa kubwa – ana kitu fulani ndani yake, ana ukuu na upekee fulani, ana uzito na thamani ambayo inakosekana kwa wengine. Badala ya kurudi nyuma, songa mbele, badala ya kuwasikiliza wapuuze, badala ya kusikiliza kejeli zao sikiliza muziki mzuri.

Kupata Div IV kidato cha nne siyo kufeli maisha, na hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kusoma sana na kufanikiwa kimaisha. Mwalimu Nyerere hakusoma sana, hakuwa profesa, lakini aliiongoza Tanzania.

Mzee Mwinyi alikuwa na digrii moja na akaiongoza Tanzania, Mzee Kikwete alikuwa na digrii moja na akaiongoza Tanzania. Wapo walioishia darasa la saba lakini leo ni watu muhimu na wenye mafanikio, unamjua Erick Shigongo? Shigongo aliishia darasa la saba tu, na akiwa na darasa la saba lake ameweza kuwaajiri mamia ya watanzania wenye digrii hadi za uzamivu.

Ishu hapa siyo Div IV, ishu ni nini unafanya baada ya kuipata. Nina mdogo wangu aliishia darasa la saba, leo ni fundi cherehani, pesa anayoingiza kwa mwezi anamshinda mwalimu mwenye digrii aliyeajiriwa kufundisha vijana.

Nina mdogo wangu mwingine aliishia darasa la saba, niongeavyo na wewe, mdogo wangu huyu ndiye mtengenezaji mkuu wa pampu na mota za vituo vya mafuta nchi nzima, anapata hela balaa.

Wanaokucheka na kukuzodoa wana lundo la ndugu ambao hawajui kama watakula kesho, mitandao ya kijamii imetufanya tuwe malimbukeni, imetufanya kazi yetu iwe ni kutukana watu mpaka watoto ambao wanapaswa kuheshimiwa.”

TOA MAONI YAKO HAPA

Recommended for you

Leave a Reply