KIMATAIFA

ALERT NEWS:Mlipuko Mwingine Wa Bomu Wajeruhi Wawili Nchini Kenya

on

Shambulizi la bomu limetokea katikati ya jiji la Nairobi Jumamosi usiku na kujeruhi watu wawili, polisi wathibitisha. Mlio mkubwa ulisikika katika eneo la Odeon, moja ya viunga vyenye shughuli nyingi na mikusanyiko ya watu wengi katikati ya jiji la Nairobi. Bomu hilo lilikuwa limefichwa ndani ya begi na kusukumwa kwa mkokoteni.

Mkuu wa polisi wa jiji la Nairobi Philip Ndolo amewaambia wanahabari kuwa, bwana mmoja mwenye asili ya Kisomali alikodi mkokoteni na kupakia begi lake, na walipofika eneo la tukio, kwenye makutano ya barabara za Tom Mboya na Latema mmiliki huyo wa begi alitoweka.

“Alimhadaa mwenye mkokoteni kwa kumwambia amsubiri akafuate kitambulisho chake ambacho alikisahau…hakurudi na baada ya muda mfupi kilipuzi kilichokuwamo ndani ya begi hilo kililipuka,”amesema bwana Ndolo.

Mlipuko huo umewajeruhi mwendesha mkokoteni na mfanyabiashara ndogondogo aliyekuwepo karibu na mkokoteni. Mlio mkubwa wa bomu hilo ulizua taharuki kubwa kwenye eneo hilo lenye stendi nyingi za mabasi ya abiria.

Shambulio hilo linakuja siku chache toka viunga vya hoteli ya kifahari ya DusitD2 kushambuliwa na kupelekea vifo vya watu 21. Tayari eneo hilo limefungwa na polisi na vikosi vya kutegua mabomu vimeshawasili eneo la tukio.

TOA MAONI YAKO HAPA

Leave a Reply