KITAIFA

Rais Magufuli Akutana Na Viongozi Wa Kidini Ikulu

on

Suala la demokrasia na uhuru wa kuzungumza Tanzania limechipuka katika mkutano wa rais John Magufuli na viongozi wa dini zote uliofanyika katika Ikulu mjini Dar es salaam.

Kiongozi huyo ameombwa kuuwaachia uhuru wa wananchi wazungumze inapowezekana ili kuruhusu demokrasia.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mchungaji wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Amani Lyimo amesema,

‘Unafanya kazi nzuri sana, lakini baba demokrasia, Watanzania wengi, wana hofu. Hata kama huambiwi na watendaji wako, wengi hawasubutu kuzungumza. Wana hofu.

‘Watu hawatachagua maneno watachagua kazi. Na kama ni mpiga kazi, tunaye, kwahiyo kama kuna uwezekano waachie wazungumze’.

Rais Magufuli, ameijibu kauli hiyo kwa kutoa hakikisho kwamba Tanzania demokrasia ipo na tena ‘ya hali ya juu’.Hatahivyo ameeleza kwamba demokrasia sio kuruhusu maandamano tu na kwamba ina mipaka yake.

‘Nyinyi ni mashahidi viongozi wa dini, mumekuwa mukisafiri katika nchi za nje, sina hakika kama mumeshuhudia maandamano na matusi kila mahali, tukienda kwa utaratibu huo, tutashndwa kuitawala nchi, tutashindwa kujenga maendeleo mengine’.

Kadhalika rais amefafanua kwamba hakuna aliyezuiwa kufanya mkutano katika maenoe yao ya uwakilishi. Ila kinachozuiwa ni viongozi kwenda kufanya fujo katika eneo la mwingine.

‘Kinachozuiliwa ni katika kudhibiti amani ya nchi hii. Mtu anatoka katika jimbo moja kwenda katika jimbo la mwenzake kutukana. Ile ni himaya ya mwingine.

Haki miliki ya pichaIKULU TZImage captionSio mara ya kwanza kwa rais Magufuli kusisitiza umuhimu wa heshima miongoni mwa wanasiasa, aliwahi kumpa salamu hizo Edward Lowassa, kiongozi wa chama cha upinzani Chadema

Ametoa wito kwa vyama vya kisiasa kufuata mfano wa namna viongozi wa dini nchini wanavyoheshimiana na kusisitiza kwamba bila ya amani mahali popote hakuna maendeleo.

Kuzuiwa kwa mikutano Tanzania

Tangu kuingia serikali ya Rais John Magufuli, wabunge na wanasiasa wanaruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara katika majimbo wanayowakilisha, na sio vinginevyo na wakati mwengine hata ruhusa hiyo pia huzuiliwa.

Hali hii wadadisi wanaona imepunguza kasi ya upinzani kuwafikia wananchi.

Kumekuwa na malalamiko kuwa demokrasia imekuwa ikiminywa Tanzania huku baadhi wakihoji kwamba mambo mengine yanafanyika kana kwamba nchi hiyo ni ya chama kimoja ilhali kuna vyama vingi vya kisiasa.

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimeshutumu hatua ya polisi nchini humo kupiga marufuku mikutano ya hadhara.

Wabunge kadhaa wa upinzani wakishtakiwa kwa makosa mbalimbali akiwemo mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo , Zitto Kabwe.

Kwa wakati mmoja hata chama cha Demokrasia na maendeleo – Chadema kilipanga kuzindua msururu wa mikutano ya hadhara nchini walioiita “Operesheni Okoa Demokrasia”.

Pamoja na mambo mengine operesheni hiyo ililenga kuishitaki serikali ya Rais John Magufuli kwa umma kuhusu maswala kama vile kufungiwa kwa kurushwa moja kwa moja kwa vikao vya bunge na aina ya uongozi wa serikali ya Rais Magufuli.

Polisi imewahi kuzuia mikutano ya upinzani katika siku za nyuma nchini humo kwa sababu tofauti ikiwemo usalama, na pia kuzuia ushawishi kwa wananchi kuvunja sheria.

Mkutano huo maalum umeandaliwa na rais Magufuli kwa madhumuni ya kukutana, kusikia kauli na kushauriana na viongozi wa kidini na madhehebu mbali mbali, kuhusu masuala wanayoyaona nchini.

Viongozi hao wa dini walipata fursa ya kuelezea matatizo yanayoyakabili maeneo kadhaa ikiwemo masuala ya kijamii, kiuchumi na hata yale ya kisiasa.Baadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria mkutano huo wameupongeza na kuhimiza zaidi ushirikiano baina yao na serikali na kueleza kwamba una nafasi ya kuleta ubora katika uongozi wa nchi.

 

TOA MAONI YAKO HAPA

Leave a Reply