ELIMU

25,532 Wapangiwa Mikopo Awamu Ya Kwanza Ya TZS 88.36 BLN

on

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwafahamisha waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019 kuwa imetoa orodha ya Awamu ya Kwanza yenye jumla ya waombaji wa mwaka wa kwanza 25,532 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 88.36 bilioni.

Akitangaza orodha hiyo leo (Jumatano, Oktoba 17, 2018) jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema kati ya wanafunzi hao, wanaume ni 16,085 na wanawake ni 9,447.

Bw. Badru ameongeza kuwa katika awamu hiyo ya kwanza HESLB pia imetoa mikopo yenye thamani ya TZS 850.35 milioni kwa watanzania wanafunzi 69wanaoendelea na masomo nje ya nchi chini ya makubaliano maalum na nchi rafiki zipatazo saba ambazo ni Msumbiji, Algeria, Cuba, Serbia, Urusi, Ukraine na Ujerumani.

Bajeti ya TZS 427.5 bilioni imetengwa kwa mikopo ya elimu ya juu 2018/2019
Katika mkutano huo, Bw. Badru ameeleza kuwa bajeti ya fedha za mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/2019 ni TZS 427.5 bilioni na tayari Serikali imeshatoa TZS 137.06 bilioni zinazohitajika wakati vyuo vinafunguliwa mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba (2018). Kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo wapatao 123,285.

Kuhusu kutangaza Awamu ya Pili
Bw. Badru amesema kuwa HESLB itaendelea kutoa awamu nyingine za orodha za wanaopangiwa mikopo kadri itakavyokamilisha uchambuzi wa orodha za wanafunzi walioomba mikopo na ambao pia wamepata na kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja ili kuhakikisha fedha za mikopo zinawafikia wanafunzi wahitaji katika vyuo walivyothibitisha.

Upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa pili na kuendelea
Akiongea katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchambuzi na Upangaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronica Nyahende amesema kuwa wanafunzi wanaoendelea na masomo na wana mikopo wataendelea kupata mikopo ikiwa wamefaulu mitihani yao na matokeo yao kuwasilishwa HESLB na vyuo husika.

Upatikanaji wa orodha kamili ya waliopangiwa mikopo
Kwa mujibu wa Bw. Badru, majina yote ya waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo katika awamu hii ya kwanza yatapatikana katika mtandao wa HESLB wa uombaji mkopo https://olas.heslb.go.tz na tovuti hii. Aidha,  majina hayo yatatumwa vyuoni kwa ajili ya kurahisisha taratibu za usajili wa wanafunzi hao.
Lengo la Bodi ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wenye sifa ya kupata mikopo katika mwaka wa masomo 2018/2019, wanapangiwa mikopo kabla vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi Oktoba, mwaka huu (2018).

Aidha, Bodi inawasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea

BONYEZA HAPA KUTAZAMA MAJINA YOTE

ADD YOUR COMMENTS