BURUDANI

Utajiri Wa P. Diddy Ni Kufuru Kwa Walala Hoi Duniani

on

MSEMO wa mtu kuwa na mkwanja mpaka anatamani kujiteka ni maarufu kwenye mitaa ya Kibongobongo. Mtu akiwa na mkwanja utasikia anasema; “Yaani nina mkwanja mpaka natamani kujiteka!” Hivyo ndivyo tunaweza kusema kwa Sean ‘Diddy’ Combs, maarufu kwa majina ya Puff Daddy au P. Diddy pia.

Jamaa ana mkwanja mpaka anatamani kujiteka! Kwa mara ya kwanza alipata kazi ya kujiingizia kipato akiwa na miaka 12 na ilikuwa ni ya kuuza magazeti nyumba kwa nyumba. Lakini kama wasemavyo Waswahili, maisha ni kama paredi, “nyuma geuka, wa kwanza anakuwa wa mwisho na wa mwisho anakuwa wa kwanza.”

Siku hizi Diddy, hapitishi magazeti hayo tena akiyauza, bali yanapita yakiwa na habari zake juu ya utajiri wake, mali anazomiliki pamoja na kazi nzuri ya muziki anayofanya.

Kwa upande wa utajiri, mshkaji huyu mzaliwa wa Harlem, New York City, Marekani ni tajiri kwelikweli. Mwaka jana Jarida la Forbes, lilimuandika kuwa ni rapa anayeongoza kwa kipato duniani akiwa na utajiri wa dola milioni 820, ambazo ni zaidi ya trilioni 1.8 za Kibongo! Mkwanja huu Diddy ameupataje?

Hili ni swali ambalo wengi wanaweza kujiuliza. Kwa wasiofahamu utajiri wa Diddy unatokana na muziki wake pamoja na biashara anazofanya na kushiriki. Diddy aliwahi kuliambia Jarida la Forbes kwamba; “Siku zote ninaelewa kwamba, kwa kuwapa wateja wangu huduma tofauti na za juu, iwe muziki, nguo au vinywaji, nitapata matokeo mazuri kutokana na kufanya kazi kwa bidii.”

Kwenye muziki mbali na mauzo ya albamu, nyimbo pamoja na ziara mbalimbali, Diddy mwenye watoto sita, anapiga mkwanja mrefu kupitia Lebo ya Bad Boy. Lakini kwa upande wa biashara anamiliki ‘brand’ ya nguo inayotumia jina la Sean John, inamuingizia takriban dola milioni 70 kwa mwaka ambazo ni zaidi ya bilioni 150 za Kitanzania. Lakini pia Diddy ana hisa kwenye makampuni ya Vodka, DeLeon Tequila na Aquahydrate water. Pesa zake anazitumiaje?

Hili nalo huwavutia wengi pia. Kufahamu ni magari ya aina gani mastaa waliofanikiwa hununua, mijengo pamoja na vitu vingine vya thamani. Sasa sikia kuhusu Diddy na tuanze na magari! Diddy anamiliki magari mengi ya kifahari tena kutoka kwenye ‘brand’ kubwa duniani. Hapa nakutajia aina tano kali zaidi.

Magari

Diddy anamiliki Phantom Drophead Coupe. Hii ni moja ya brand inayotengenezwa na Kampuni la Kingereza liitwalo Rolls Royce na Diddy alilinunua dola 444,000 ambazo zinachezea kwenye shilingi bilioni 1 za Kibongo.

Anamiliki pia Lamborghini Gallardo Spyder lenye rangi ya silva ambalo alilinunua dola 300,000, ambazo ni zaidi ya milioni 681 za Kibongo. Mbali na gari hilo Diddy anamiliki pia Maybach 57 ambayo inajulikana pia kama Benz Maybach, anamiliki Jeep Wrangler Unlimited pamoja na Corvette.

Nyumba

Diddy anamiliki pia nyumba kali na za thamani kubwa katika miji tofauti Marekani. Kwa miaka kadhaa huko nyuma alikuwa akiishi New York, lakini miaka ya hivi karibuni amehamia Los Angeles, kwenye mjengo wake alionunua kwa dola milioni 40 ambazo ni zaidi ya bilioni 90 za Kibongo!

Mjengo huo unaopatikana kwenye kilima cha Holmby, unatajwa kuwa na zaidi ya ukubwa wa ‘square-foot’ 17, 000 ukiwa ndani na bwawa la kuogelea, studio, kiwanja cha michezo, na vitu vingi vinavyomfanya aishi maisha ya ‘luxury’ pamoja na familia yake.

Meli

Kama haitoshi, Diddy mkwanja wake mwingine amewekeza majini kwa kununua meli ambayo ‘some-times’ huitumia kwa misele ya bata pamoja familia yake.

Meli hiyo anayomiliki inaitwa Oasis, aliinunua dola milioni 72, ambazo ni zaidi ya bilioni 163 za Kibongo, kutoka kwa Mwenyekiti Msaidizi wa Mtandao wa Google, Eric Smidt.

Haya ndiyo maisha ya P. Diddy, pamoja na baadhi ya mali zake. Katika suala zima la mafanikio mara nyingi amekuwa akiwaambia watu wapambane ili kufikia ndoto zao na kuishi wanavyotaka. Lakini huwa ana utani wake pia ambapo huwa anasema; “Kama huwezi kufanya mambo ya kunivutia nikajifunza kutoka kwako, endelea kuniombea nifanikiwe zaidi na zaidi!”

ADD YOUR COMMENTS

You must be logged in to post a comment Login