KIMATAIFA

Utata Unaendelea Juu Ya Kifo Winnie Mandela Huko Afrika Ya Kusini!

on

MKE wa zamani wa Nelson Mandela, Winnie Mandela ambaye alipigana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini kifo chake kilichotokea Aprili 2 mwaka huu kimezua mjadala nchini mwake, namna ambavyo mwanaharakati huyo anastahili kukumbukwa.

Kwa upande wa viongozi wa jadi pamoja na wafuasi wake, wanataka Winnie akumbukwe kama mwanamke asiyekuwa na hatia, shujaa na mpambanaji huku wengine, haswa wale ambao bado wapo katika mapambano ya awali wakiwa chini ya mwamvuli wa watu weupe wanataka Winnie Mandela kukumbukwa kama mtu mbaya sana na aliyetenda uasi.

Lakini kwa mtu yeyote ambaye anataka kumuelewa vizuri Winnie Mandela anapaswa kurejea historia na kuona namna ambavyo alinyanyaswa,kuaibishwa na kuteseka wakati wa mfumo wa ubaguzi wa rangi enzi ya utawala wa Makaburu.

Winnie alikuwa mpigania uhuru, aliyeleta mapinduzi kwa kuwa mpambanaji wa ubaguzi wa rangi, hakuwa mwanaharakati wa kushika silaha na kutegemea mashabiki wa mitandaoni .

Mume wake wa zamani, Nelson Mandela alimwachia watoto wadogo wawili wa kike kuwalea wakati alipofungwa kifungo cha maisha gerezani mwaka 1962.

Winnie kuitwa mwanaharakati ni haki yake kwa kuwa ni mwanamke aliyewahi kukamatwa na kuwekwa gerezani akiwa na nguo zake za kulalia tu, huku polisi wakiwazuia ndugu zake kwenda kumuona na kuzuiwa kuwaona watoto wake.

Mwaka 1969, Winnie alifungwa gerezani kwa muda wa siku 491, na hakupata msaada hata wa pedi wakati alipokuwa katika siku zake, huo ukatili mkubwa walimfanyia Makaburu. Gereza alilowekwa halikuwa la kawaida, ila maalum kwa ajili ya kumtesa.

Mateso aliyoyapata gerezani yaliandikwa katika kitabu kiitwacho “491 Days”, kinachoelezea kelele ya mwanamke aliyekuwa anapigwa na kuteswa gerezani.

Baadaye wakati ambapo viongozi wengi walipokuwa wanafungwa jela,.Winnie alikuwa mstari wa mbele katika kuongoza harakati hizo akiwa pamoja na hayati Mandela.

Kiufupi ni kwamba Winnie Mandela aliamua kuongoza mapigano ya kutetea watu weusi. Alipobainika kuwa ana ushawishi mkubwa, Winnie alihamishwa katika makazi yake yaliyokuwa katika mji wa biashara wa Johannesburg, kwenda kukaa katika mji mdogo wa Brandfort ambayo ilikuwa ngome imara ya watu weupe.

Hakuruhusiwa kupokea wageni ingawa alikuwa anaweza kusafiri kila siku kwenda posta kupiga simu, ili kuuambia ulimwengu juu ya mfumo wa ubaguzi wa rangi ulivyo mbaya.

Tangu kifo chake kitokee siku ya Jumatatu ya Aprili 2 mwaka huu, kile kilichoandikwa na watu wengi katika mitandao ya kijamii, kinaonesha wazi kuwa kuna baadhi ya watu hawafahamu historia yake.

Kuna wengine wamezungumzia juu ya urembo wake na wengine jitihada zake katika kutetea nchi yake.Aidha Winnie pia hakuwa mkamilifu, alikuwa na makosa yake pia kama binadamu.Aliwahi hukumiwa kwa kosa la udanganyifu na alikamatwa kwa kosa la utekaji nyara.Anatarajiwa kuzikwa Jumamosi ijayo, Aprili 14 mwaka huu.

ADD YOUR COMMENTS

You must be logged in to post a comment Login