BannerFans.com

AFYA

Arusha: Wanaume wagoma kwenda kliniki na wake zao

on

Kampeni  ya kuwataka wanaume waongozane na wenza wao wajawazito kiliniki kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu  kuhusu afya ya uzazi sambamba na uzazi wa mpango, inaelekea kukwama katika jiji la Arusha na hivyo kutishia kinamama kukosa matibabu.

Katika kampeni hiyo  ambayo mama anayeshindwa kufika na mumewe kiliniki hunyimwa  cheti ili  kuweka mkazo suala hilo.

Kutokana na hali hiyo, suala hilo limesababisha wajawazito  jijini Arusha  kubuni mbinu mpya ya kukodi vijana kuwasindikiza hospitali.

Naibu Meya wa Jiji la Arusha ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya  madiwani wa kupambana  na Ukimwi, Viola Likindikoki alitoa taarifa hiyo juzi wakati akiwasilisha taarifa yake ya robo tatu ya mwaka uliomalizika Januari mwaka huu.

Amesema mgomo wa wanaume wengi katika jiji la Arusha, unawapa  wakati mgumu  wanawake wanaotakiwa kuambatana na waume zao kliniki kutokana na kuwakatalia hivyo kuwalazimu kukodi vijana ili mradi tu waonekane na waume zao ili wapatiwe huduma.

Amewataka viongozi wote wa ngazi ya kata na vijiji kuungana kusisitiza umuhimu wa watu wote kuhudhuria kliniki au kupima maambukizo  kwa lengo la kutambua hali halisi na kupata msaada wa haraka.

“Unajua wafadhili waliokuwa wanafadhili hizi kampeni za kutokomeza Ukimwi wengi wamejitoa, hivyo sisi viongozi tunaowawakilisha wananchi tusibweteke bali iwe chachu ya sisi kupambania maisha ya wananchi wetu.”

Akizungumza na waandishi wa habari, Diwani wa Ngarenaro, Issaya Doita amesema wanaume wengi wanakimbia kuongozana na wanawake hao kutokana na wengi siyo waume zao au wanabanwa na shughuli nyingi za kikazi

“Huu mji ni wa utalii, una pilikapilika nyingi za kusaka uchumi wa nyumbani hivyo wanaume wengi wanakwambia wana kazi nyingi hawawezi kwenda kukaa kliniki halafu jioni walale njaa, lakini sababu nyingine wanayotuambia baadhi yao si wake zao bali ni ‘mchepuko’ hivyo wanaogopa taarifa zao kuwekwa,” amesema Doita.

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia amesema  watahakikisha wanawake kliniki wanakuwa na waume zao la sivyo watafuatilia taarifa zao na watakaobainika kukodi vijana wataumbuliwa.

ADD YOUR COMMENTS

You must be logged in to post a comment Login